Ndugu walimu, mazingira yenu ya kazi ni magumu

Nakumbuka siku moja nilikuwa nasubiri kikao ofisini kwa afisa elimu wilaya. Ilikuwa mwaka 2004, wilaya ya Kilolo ilikuwa mpya. Enzi zile, hata ukifika makao makuu ya wilaya, ni kama uko kijijini ndani kabisa. Kila kitu kilikuwa bado. Nje ya ofisi, eneo lilijaa walimu wapya wanaosajili na kuambiwa vituo vya kazi. 

Niliongea na dada moja kijana*, anisamehe nimemsahau jina lake. Tumwite Chiku. 

Chiku alitoka mkoa mwingine, na alikuwa na wasiwasi atapelekwa wapi. Ametajiwa jina la kijiji, lakini bado hajui kama habari ni nzuri au vipi. "Siyo mbali sana" akasema mwenzangu - mfanyakazi mstaafu wa idara ya elimu. "Kwa basi ni kama masaa 8, halafu unatembea kilometa 30." 

Yaani. Sijui Chiku aliendaje au alikaa muda gani. Mwenyewe unajua angetegemea mazingira gani akifika. Kijiji ambacho hakifikiki kwa basi kitakuwa na huduma gani? Kakituo ka afya? Mtandao, umeme, maji? Nyumba za walimu, vipi? Hata chakula inaweza kuwa shida.  Inategemea wenyeji wamechangamka kiasi gani. 

Madiwati kama yapo, yanakarabatiwa inapobidi? Walimu wa kutosha? 

Je mwalimu anaweza kufundisha vizuri kwa mazingira hayo? Ndiyo anaweza!

Anaweza kuwa mwalimu bora Tanzania na hata dunia nzima. Anachohitaji kiko kichwani na moyoni. Ujasiri, ubunifu, utaalam, upendo, elimu, ushirikiano, na kujitambua. 

Of course atahitaji support. Lakini kwanza tukubali kwamba inawezekana. 

Je, tukimpa moyo na mbinu kwa njia ya intaneti, mnaonaje? Hata kijijini kwake, ilivyo mbali, anaweza kubadilisha maisha ya wanafunzi wake. 

Na wewe mwalimu msomaji, uko mjini na mazingira yako ya kazi ni nafuu lakini unataka kujiendeleza na kuwa mwalimu bora.

Basi karibu sana. Hii blog ni kwa ajili yako. Natumaini utapata mawazo mapya mengi hapa, tutaelimishana na kupeana moyo.

 

*Dada - kama kwa bahati nzuri unakuja kusoma jarida hii, naomba uwasiliane na kutuambia stori yako! 

Naomi Rouse